You are currently viewing Samia ataja sababu deni la Taifa kuongezeka

Samia ataja sababu deni la Taifa kuongezeka

Rais Samia Suluhu Hassan amesema hadi mwezi Mei, 2025, deni la Serikali lilifikia Sh107.7 trilioni, kati ya hilo la nje ni Sh72.94 trilioni na ndani ni Sh34.76 trilioni.

Kwa mujibu wa Rais Samia, kuongeza kwa deni hilo kumetokana na kupokelewa kwa fedha za mikopo mipya na ya zamani ambayo mikataba yake iliingiwa na Serikali zilizopita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Rais Samia ameeleza hayo leo Ijumaa Juni 27,2025 wakati akihutubia Bunge jijini Dodoma.

“Ni vema tukafahamu kuwa mkopo unaweza kusainiwa leo, lakini fedha husika zikaanza kupokelewa baada ya maandalizi ya mradi kukamilika au mradi kuanza. 

“Hivyo ili liwe deni au mkopo uingie kwenye deni la Serikali ni lazima Serikali iwe imepokea fedha hizo, huduma au vifaa tulivyokubaliana,” amesema Rais Samia.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na kusaini mikopo mipya, imeendelea kupokea fedha za mikopo iliyosainiwa katika vipindi tofauti na kuongeza kiasi cha deni la Serikali.

“Kwa mfano awamu ya sita imepokea Sh11.3 trilioni ikiwa ni mikopo iliyosainiwa na awamu zilizopita. Sababu nyingine za kuongezeka kwa deni la nje ni kuimarika kwa dola ya Marekani dhidi ya Shilingi ya Tanzania,” amesema.

Amesema Machi 2021 kiwango cha kubadilisha Dola kilikuwa Sh2,298.5 wakati Machi,2025 ilikuwa Sh2,650, hivyo iwapo deni la Serikali litatajwa kwa Shilingi za Tanzania lazima lionekane limeongezeka.

“Kwa mfano deni la Serikali kwa sasa limeongezeka kwa zaidi ya Sh3.9 trilioni kutokana na kiwango cha kubadilisha fedha. Hatua hii ya kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya dola ya Marekani isichukuliwe kama hatua hasi bali ilikuwa hatua muhimu ya kukabiliana na mtikisiko wa uchumi wa dunia,” amesema Rais Samia.

Kuhusu mwenendo wa ulipaji wa deni la Serikali, Rais Samia amesema yamekuwa yakiongezeka kutoka Sh8.22 trilioni mwaka 2020/21 hadi kufikia makadirio ya Sh14.2 trilioni kwa mwaka 2025/2026. Kutokana na kuiva kwa mikopo ya muda mrefu na ile yenye masharti ya kibiashara iliyokopwa katika awamu zilizopita kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Rasi Samia amesema kuongezeka kwa malipo ya deni hasa ya nje kumesababishwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya viwango vya riba.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa nchi, mabadiliko hayo, yamesababisha baadhi ya nchi hasa zinazoendelea Afrika kushindwa kulipa madeni.

Leave a Reply