Rais Samia Suluhu Hassan ameziagiza Wizara za Uchukuzi na Viwanda na Biashara kuanza kutoa huduma zote za kibandari katika Bandari Kavu ya Kwala ili kurahisisha shughuli za usafirishaji kuanzia tarehe 4 Agosti, 2025.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo leo wakati wa uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala (Kwala International Logistics Centre) mkoani Pwari, ambapo amesema ni hatua ya kihistoria itakayopunguza gharama za usafirishaji, kuondoa msongamano wa malori katika Jiji la Dar Salaam, na kuchochea ukuaji wa uchumi, uwekezaji wa viwanda na ajira kwa Watanzania.

Aidha, Rais Dkt. Samia amesema kuwa uzinduzi wa kituo hicho utarahisisha shughuli za uchukuzi na kupanua wigo wa biashara kwa Watanzania na nchi jirani.
Ameongeza kuwa kituo hicho kinalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa ni maandalizi ya ushiriki kamili wa nchi katika Eneo Huru la Biashara la Afrika (A{CFTA).
“Bandari Kavu ya Kwala itarahisisha usafirishaji wa mizigo ya nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Burundi, Rwanda na Malawi na kuongeza mvuto wa Bandari ya Dar es Salaamn katika ushindani wa kikanda,” alibainisha Rais Dkt. Samia.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amezindua rasmi safari za mizigo za treni ya umeme ya SGR, ambapo amesema kuwa hatua hiyo muhimu itakayobadili mfumo wa uchukuzi nchini ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupunguza gharama za usafirishaji, kupunguza uchakavu wa barabara na kulinda mazingira.
Rais Dkt. Samia pia amesema Serikali imewekeza Shilingi Bilioni 330.2 kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa 1430 ya mizigo ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama kwa wafanyabiashara.
Pia ametoa wito kwa sekta binafsi kutumia fursa ya uwepo wa reli hiyo kuwekeza katika usafirishaji wa mizigo na abiria, ikiwemo kununua vichwa na mabehewa yao wenyewe.
Halikadhalika, Rais Dkt. Samia aliweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Kongani ya Viwanda ya Kwala (Kwala Industrial Park) inayotarajia kuwa na viwanda 200 itakapokamilika, ambapo viwanda saba tayari vimekwishaanza kazi na vitano vipo katika hatua ya ujenzi.
Akizungumzia fursa za ajira, Rais Dkt. Samia amewataka wananchi wa mkoa wa Pwani na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa hizo, ikiwemo kuanzisha biashara ndogondogo na huduma zinazozalishwa na mradi huu, akitaja kuwa ajira 50,000 za moja kwa moja na 150,000 zisizo za moja kwa noja zitazalishwa kutokana na viwanda 200 vitakavyojengwa katika Kongani hiyo ya Viwanda.