Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, amesema Mkoa wa Kigoma hautakuwa tena mwisho wa reli bali itakuwa mwanzo wa kufunguka kwa fursa biashara na uwekezaji.
Dkt Samia ameeleza hayo leo Jumatatu Julai 20,2026 wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) kutoka Tabora hadi Kigoma, pamoja uzinduzi wa meli nne za mizigo katika ziwa Tanganyika.
Amesema miundombinu ya reli, meli, barabara na uwanja wa ndege inayoendelea kutekelezwa na Serikali inakusudia kuunganisha shughuli za kiuchumi za Mkoa wa Kigoma na masoko ya ndani ya nje ya nchi.
“Kigoma itastawi na kunawiri, leo tumewekea jiwe la msingi la kipande cha reli ya kisasa cha Kigoma kwenda Tabora chenye urefu wa kilomita 506 ujenzi wake utagharimu Sh 7.4 trilioni,”
Dkt Samia amesema ujenzi wa reli hiyo ukikamilika utaungakisha Kigoma na mikoa mingine ya Tabora, Dodoma na Dar es Salaam pamoja na mtandao mwingine wa reli ya Mwanza.
