Rais Samia Suluhu Hassan, amesema ametimiza ndoto ya Baba wa Taifa wa Julius Nyerere, kwa kukamilisha ujenzi wa majengo ya wizara, taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali wa Mtumba jijini Dodoma.
Amesema mwaka 2021 wakati akichukua uongozi wa nchi, mradi huo ulikuwa na majengo ya awali ya kujishikiza, hivyo yeye pamoja na viongozi wenzake waliongeza jitihada za ukamilishaji wake.
Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa wakati wa uzinduzi wa majengo ya wizara, taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali wa Mtumba jijini Dodoma.
“Pamoja na majengo ya awali ya kujishikiza, tuliamua kuendeleza mradi wa ujenzi huu wa majengo ya Serikali kwa kujenga majengo ya kudumu ya ghorofa, barabara za lami na miundombinu mengine wezeshi,” amesema na kuongeza kuwa;
“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kutimiza tulioyakusudia, hakika tunapaswa kujipongeza sote Watanzania kwa mafanikio makubwa haya,” amesema Rais Samia.
