Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan, amesema dhamira yake ni kujenga barabara za kiwango cha lami katika wilaya zote ili kuziunganisha na makao makuu ya mikoa.
Mbali hilo, Dkt Samia ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, amewaihidi Watanzania kujenga pia madaraja ili kupunguza changamoto mbalimbali zinazotokana na kutokuwepo kwa vivuko.

Dkt Samia ameeleza hayo Jumatano Septemba 3,2025 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kampeni za kusaka kura, uliofanyika Vwawa mkoani Songwe.
“Nataka kusema madaraja yote na barabara ndani ya miaka mitano inayokuja tunakwenda kujenga.Lengo letu kuunganisha wilaya zote na makao makuu ya mikoa kwa kiwango cha lami,” amesema na kuongeza kuwa :
“Hii kazi inaendelea kufanyika, tutaendelea kuifanya hadi tuhakikishe wilaya zote Tanzania zimeunganishwa kwa barabara za lami na makao makuu ya mikoa,”amesema Dkt Samia.
Kuhusu umeme, Dkt Samia amewahakikishia wananchi wa Songwe kuwa kazi kubwa imefanyika kujenga njia ya kilovati 730 ya kusafirishia umeme kutoka Iringa hadi mkoa huo.
“Kati ya kilovati 730, kilovati 400 zitatumika katika mikoa mitatu ukiwamo wa Songwe, zilizobaki tutauzwa kwa majirani zetu (Zambia). Huu ndio mpango wetu ndani ya mitano, mbali na kuiunganisha Songwe katika gridi ya Taifa, lakini tunahitaji kujenga njii hizi,”