You are currently viewing TARURA yakamilisha ujenzi wa daraja la mto Kalambo

TARURA yakamilisha ujenzi wa daraja la mto Kalambo

Na Mwandishi Wetu, Rukwa

Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekamilisha ujenzi wa daraja la mto Kalambo lenye urefu wa mita 80 pamoja na ujenzi wa barabara unganishi ya Sopa-Mtutumbe-Kasitu kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya shilingi bilioni 5.142 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Chacha Moseti ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo kwaajili ya ujenzi wa daraja la mto Kalambo ambalo limenufaisha wananchi wa kata za Sopa na Pombwe kusafirisha mazao yao na kuyafikisha sokoni kwa urahisi.

“Daraja hili limesaidia wananchi kiuchumi, wananchi wa hapa wanajishughulisha na kilimo cha maharage, mahindi, alizeti pamoja na shughuli za ufugaji ambapo kwa sasa wanasafirisha mazao yao kwenda Sumbawanga na Tunduma bila shida yoyote”, alisema.

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nondo, Tedd Tilundi amesema hapo awali walikuwa wanavuka kwenye daraja la miti, kipindi cha mvua mto ulikuwa unajaa maji, watu wengi wamepoteza maisha, pikipiki zimesombwa sana na maji, lakini sasa hivi wanaishukuru serikali kwa kuwajengea daraja hilo ambalo limerahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.

’’Tunaishukuru Serikali, daraja hili limefungua soko, sasa tunapeleka mazao yetu wilayani Matai, wengine hatukuamini kama tungejengewa daraja na lingeisha, tunaishukuru serikali kwa kutujengea daraja hili kwani njia hii inafika hadi Zambia”, alisema.

Kwa upande wake, Emmanuel Justin mkazi wa kijiji cha Nondo, ameishukuru serikali kwa uwepo wa daraja hilo ambalo limewaletea mafanikio makubwa, shida kubwa ilikuwa ni uvushaji wa mazao na watu, kipindi cha masika wajawazito walikuwa wanapata shida kwenda zahanati ambayo ipo kijiji cha ng’ambo Kasitu, lakini sasa hivi daraja hilo limewasaidia wanasafirisha mazao yao soko la Kasanga bila shida wanaishukuru serikali kwa kusikiliza kilio chao cha muda mrefu.

Wakati huo huo mkazi wa kijiji cha Kasitu, Geofrey Raphael ameishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo limefungua mawasiliano ya vijiji vya Nondo na Kasitu, kwa sasa wanasafirisha gunia moja lenye mazao kwa shilingi 3000 tofauti na kipindi cha nyuma walikuwa wanasafirisha gunia moja shilingi 8000.

Mkazi wa Kijiji cha Nondo, Ester Litungulo ameishukuru serikali kwa kutengeneza daraja hilo kwani kipindi cha nyuma wanafunzi walikuwa wanashindwa kuvuka mto huo kwenda shule lakini sasa hivi wanavuka bila shida na wanafika shule kwa wakati.

Leave a Reply