Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan, amewaomba wakulima wa mbaazi, choroko na dengu kuwa wavumilivu kuhusu mauzo ya zao hilo, akiwaahidi bei nzuri inakuja.
Dkt Samia ameeleza hayo leo Jumatano Septemba 10,2025 akiwaaga wananchi wa mkoa wa Singida eneo la Misigiri wilayani Iramba, wakati akihitimisha ziara ya kampeni katika mkoa huo, kabla ya kuendelea mkoa wa Tabora.

Katika maelezo yake, Dkt Samia amesema mwaka huu, mazao hayo yamezalishwa kwa wingi katika mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania, kutokana na hilo bei za bidhaa hizo zimeshuka
Hata hivyo, Dkt Samia amewatoa hofu wakulima wa mazao hayo nchini, akisema Serikali ipo katika mazungumzo na India ambayo ndio mnunuzi mkubwa wa bidhaa hiyo, ili kuweka utaratibu wa kuyanunua kwa bei ya kuridhisha.
“Nataka niwahakikishie mazungumzo yetu hayashuka chini ya asilimia 60 ya bei ya dunia. Tunakwenda vizuri, tutafika pahali pazuri na watakuja kununua dengu na mbaazi zetu, lakini bei hataishuka chini asilimia 60 ya bei ya dunia,”
“Kwa hiyo ndugu zangu naomba muwe wastahimilivu, tupeni muda kuanzia asilimia 60 hadi asilimia 75 , tunakwenda kupata bei nzuri, tupo katika mazungumzo, tupeni muda ili tutumize hili,”amesisitiza Dkt Samia.
Kuhusu upatikanaji wa maji safi kwenye baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Singinda, Dkt Samia amewahakikishia wananchi wa mkoa huo kulitatatua suala, akiwaomba kumpa ridhaa ya kumchagua kwa nyingi.
“Tukimaliza uchaguzi hapa, ule mradi kubwa na mkitupa ridhaa ya kuongoza Serikali nitamkaba Mwigulu (Dk Nchemba-Waziri wa Fedha) azitafute fedha ili mradi mkubwa kutoka ziwa Victoria upite hapa hadi Dodoma ili kutatua changamoto,”
“Sasa Mwigulu atazipata wapi fedha, mimi na yeye tutajua,” amesem Dkt Samia huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliofurika kumsikiliza.