You are currently viewing Serikali yafuta usajili meli iliyokamatwa na dawa za kulevya

Serikali yafuta usajili meli iliyokamatwa na dawa za kulevya

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amekiri kupokea taarifa za kukamatwa kwa meli ya FMS Eagles yenye bendera ya Tanzania, inayodaiwa kukutwa na tani 6.6 za dawa za kulevya nchini El Salvador.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Msigwa amesema kwa mujibu wa takwimu za usajili, meli hiyo ilisajiliwa Zanzibar, na kwamba tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufuatia tukio hilo.

Ameeleza kuwa baada ya kupokea taarifa za kukamatwa kwa meli hiyo Februari 17, 2026, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilichukua hatua ya haraka kufuta usajili wa meli hiyo Februari 18, 2026, hatua inayomaanisha kuwa kwa sasa meli hiyo haina usajili wa Zanzibar.

Mbali na kufuta usajili, serikali hiyo imeanza kuwatafuta wamiliki wa meli ili kubaini chanzo cha tukio hilo. Pia, kampuni inayohusika imepigwa faini ya dola za Marekani 20,000 kwa mujibu wa taratibu za Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO).

Aidha, Msigwa amesema serikali inaendelea kufanya mawasiliano kupitia Wizara ya Mambo ya Nje kwa lengo la kuondoa au kuepusha athari zozote za utambuzi wa kimataifa zinazoweza kujitokeza kufuatia tukio hilo.

“Ni kweli meli hiyo ilisajiliwa Tanzania, lakini ni meli ya kigeni iliyokuwa ikifanya kazi nje ya nchi. Kutokana na kuvunja taratibu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeanza kuchukua hatua, na baadaye itatoa taarifa rasmi kuhusu hatua nyingine zilizochukuliwa,” amesema Msigwa.

Ameongeza kuwa meli hiyo haikuwa na Mtanzania hata mmoja bali ilikuwa na wageni pekee.

Leave a Reply