You are currently viewing Serikali yakanusha madai ya kuzuiwa wafanyakzi wasio Wazanzibar

Serikali yakanusha madai ya kuzuiwa wafanyakzi wasio Wazanzibar

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili Zanzibar, Hamza Hassan Juma amesema hakuna mwananchi wa Tanzania Bara, aliyezuiwa kuingia kazini kwa kigezo cha kutakiwa kuwa na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Juma ameeleza hayo leo Ijumaa Juni 19,2026 akijibu upotoshwaji unaofanyika kupitia picha jongefu inayowaonesha vijana ambao ni vibarua wa hoteli, ujenzi na wafanyakazi wa hoteli wanaodai wamezuiwa kutoingia kazini kwa sababu ya kutokuwa kuwa na vitambulisho hivyo.

“Naomba kukanusha taarifa hiyo, si kweli ni uzushi. Wale ni wafanyakazi wa hoteli ya Jaz, ambayo wiki mwanzoni kulitokea wizi na meneja wa hoteli aliagiza asiingie mtu yeyote asiyekuwa na kitambulisho bila kujali cha Mzanzibari au Mtanzania,” ameeleza Juma.

Kwa mujibu wa Waziri Juma, kijana aliyerekodi ‘clipu’ amechukua mkundo wa sasa kuhusu tuhuma za madai ya ubaguzi baina ya Zanzibar na Tanzania Bara ili kuongeza taharuki.

Amefafanua kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, haijamzuia mtu yeyote kufanya kazi, na kwamba haikubaliani na watu wazululaji bali wote wanaoishi visiwani humo wanafanya kazi za halali.

“Tayari uongozi wa hoteli ya Jaz wametoa taarifa polisi Chwaka kuhusu wizi huo na jeshi linaendelea na uchunguzi wa kubaini mfanyakazi gani au nani aliyehusika na wizi huo,” amesema nakuongeza kuwa;

“Ndugu wananchi tuendelea na mshikamano baina ya Tanzania Bara na Zanzibar na Muungano wetu huu, kuna watu wanautia chokochoko lakini hautavunjika kwa sababu tupo pamoja,” amesema Waziri huyo.