You are currently viewing Serikali yaongeza Sh Bilioni 10.5 kupanua fursa za mitaji kwa machinga

Serikali yaongeza Sh Bilioni 10.5 kupanua fursa za mitaji kwa machinga

Serikali imeongeza mtaji wa Mfuko wa Machinga kwa Sh bilioni 10.5 katika mwaka wa fedha 2025/26 ili kupanua fursa za mitaji kwa wafanyabiashara wadogo nchini.

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema nyongeza hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha shughuli za uchumi wa wananchi na kuwezesha wafanyabiashara wadogo kukuza biashara zao.

“Serikali imeongeza mtaji wa Mfuko wa Machinga kwa Sh bilioni 10.5 ili kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kupata mitaji ya kuendesha na kupanua shughuli zao za kiuchumi,” amesema Waziri Omar wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/27 bungeni leo Juni 11, 2026.

Hatua hiyo inakuja wakati sekta ya biashara ndogo ndogo ikiendelea kuwa chanzo muhimu cha ajira na kipato kwa maelfu ya Watanzania, hususan vijana na wanawake katika maeneo ya mijini na vijijini.

Nyongeza ya fedha katika mfuko huo inatarajiwa kuongeza uwezo wa wafanyabiashara wadogo kupata mikopo nafuu na kuboresha mazingira ya kufanya biashara, sambamba na jitihada za Serikali za kukuza uchumi jumuishi.

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuwawezesha wajasiriamali wadogo kama sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji, ajira na kipato cha wananchi katika ngazi zote za uchumi.