Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam
Baadhi ya wananchi na wanafunzi wamepongeza maboresho ya kituo cha huduma ya wateja cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambacho kinataja kuwarahisisha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi wa taasisi hiyo.
Hayo yamebainishwa na baadhi ya wananchi hao ikiwa ni siku chache baada ya mamlaka hiyo kutangaza kufanya maboresho makubwa ya kituo chake cha huduma kwa wateja maarufu ‘Call Center’ na kueleza kuwa kitakidhi matarajio ya watanzania wengi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam mmoja wa wanafunzi hao, Atupele Mwakalinga ambaye anasoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema maboresho hayo yatasaidia sana wanafunzi hasa wale wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Amesema mojawapo ya vigezo vya kupata mkopo ni kuwa na namba ya NIDA jambo ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa wanafunzi hao.
“Wanafunzi wengi wanashindwa kupata mikopo ya elimu ya juu kutokana na kutokuwa na namba wala kitambulisho cha NIDA, ujio wa namba hii ya huduma kwa wateja itasaidia wanafunzi wengi kupata namba au kitambulisho cha NIDA na kupelekea kupata mikopo,” alisema Mwakalinga.
Yassin Chuma ambaye ni mjasiriamali kutoka Mabibo Sokoni alisema kuwa maboresho yaliyofanywa yatatoa wigo kwa wananchi wengi kujua taarifa zao binafsi zinazofanyiwa kazi na mamlaka hiyo.
Amesema kwa wafanyabiashara wakiwemo wajasiriamali wadogo wadogo, maboresho hayo yamekuja wakati muafaka kwa sababu ya uhitaji mkubwa wa namba ya NIDA kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
“Maboresho haya yamefanyika wakati sahihi ambao watu wengi hawana namba wala vitambulisho vya NIDA, kwa hiyo uwepo wa namba hii utasaidia hata kwa wale ambao hawajajiandikisha wataitumia kwa kupiga simu kwa watoa huduma na kuhudumiwa bila kwenda ofisi za mamlaka hiyo,” alisema Chuma.
Naye Anna Msuya mkazi wa Kigamboni alisema maboresho haya yatapunguza urasimu uliokuwepo awali kupata namba au vitambulisho kutokana na maofisa au makawala wachache waliokuwa siyo waaminifu.
“Siku hizi mambo yanakwenda kidijitali, kwa hiyo maboresho haya ni muhimu na hivyo yataleta mageuzi makubwa ndani na nje ya NiDA pia kuongeza Imani kwa chombo hicho,” alisema Msuya.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Msemaji na Afisa Habari Mkuu wa NIDA, Geofrey Tengeneza alibainisha kuwa mpaka sasa wamezindua mfumo wa usajili kupitia mtandao, ambapo mwananchi anaweza kuanza hatua za mwanzo za usajili kupitia tovuti yao na kumuwezesha kufuatilia na kufahamu nafasi ya maombi yake yalipofikia.
Alisema kuwa maboresho hayo ni pamoja na mabadiliko ya namba za simu, ambapo kuanzia Oktoba 28, 2024, namba itakayokuwa inatumika ni 023221 0500 ya TTCL na namba nyingine za mitandao mbalimbali zilizokuwa zinatumika hapo awali hazitatumika tena baada ya tarehe hiyo.
Mbali na uzinduzi huo wa namba maalumu itakayotumika kuwasiliana na wateja wake, Nida imejipanga kuongeza idadi ya watoa huduma katika hicho cha huduma kwa wateja ili kurahisisha mawasiliano na wateja.
“Kuna baadhi ya changamoto zitatatuliwa wakati huo huo na wahudumu wetu mwananchi anapopiga simu na mengine yatapokelewa na kujibiwa pia kulingana na shida ya mtu,” alisema.
Alisema NIDA inalenga kila simu ya mteja inayopigwa iweze kupokelewa ndio maana tumepanga kuongeza idadi nzuri ya watoa huduma kwa wateja ili kila simu i iweze kupokelewa” alibainisha Tengeneza.
Tengeneza aliwaasa wananchi wote waliokidhi vigezo waende kwenye ofisi za mamlaka hizo zilizopo jirani nao waweze kijiandikisha na kupata vitambulisho vyao kwani zoezi hilo ni endelevu na ni haki ya kila mwenanchi mwenye sifa ya kupata kitambulisho.