You are currently viewing Serikali yatangaza hatua kuhakikisha mafuta yanapatikana

Serikali yatangaza hatua kuhakikisha mafuta yanapatikana

Serikali imewahakikishia wananchi uwepo wa akiba ya mafuta ya kutosha nchini, huku ikijidhatiti kufanya kila linalowezekana kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa wananchi.

Hayo yameelezwa leo, Jumatatu Machi 23, 2026 na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, katika kikao na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo zinazohusika na sekta ya mafuta.

“Hatutarajii kuona mfanyabiashara yeyote akificha mafuta kwa kisingizio cha kusubiri bei kupanda. Nchi ina akiba ya kutosha na Serikali ya Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan, imejipanga kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bila vikwazo,” amesema.

Ameagiza kuundwa kwa kamati maalumu ya kufuatilia mwenendo wa uingizaji wa mafuta nchini, na kufanya jitihada zote za kuhakikisha Tanzania haikosi nishati hiyo.

Timu hiyo, ametaka ihusishe wataalamu kutoka Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) Ewura, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na vyombo vya ulinzi na usalama.

Hatua hizo za Serikali zinalenga kuepusha nchi kukabiliwa na uhaba wa mafuta, kutokana na vita inayoendelea Mashariki ya Kati, ikihusisha mataifa ya Marekani na Iran, ukanda ambao ni kitovu cha uzalishaji na usafirishaji wa mafuta duniani.

Tayari vita hiyo imeshazalisha hatari ya kufungwa kwa njia ya usafirishaji wa mafuta ya Strait of Hormuz, inayounganisha Ghuba ya Uajemi na masoko ya dunia. Takribani asilimia 20 ya mafuta yote duniani hupita hapo kila siku.

Leave a Reply