Kufuatia vikwazo vya Ulaya dhidi ya mashirika matatu ya ndege ya Iran, Shirika la ndege la Iran Air, limetangaza kusitisha safari zake zote za ndege kuelekea nchi za Ulaya.
Iran Air ilikuwa kampuni ya mwisho ya Iran kuwa na safari za ndege kuelekea Ulaya, hasa kuelekea Ufaransa na Ujerumani. Imeamua kusitisha safari zake zote za ndege kwa sababu ya vikwazo vya Ulaya.
Shirika lingine la ndege kutoka Iran la Mahan Air lilisitisha mapema safari zake za ndege kuelekea nchi za Ulaya.
Umoja wa Ulaya ulipitisha vikwazo hivi vipya kwa kuishutumu Iran kwa kutumia mashirika yake ya ndege kupeleka makombora kwa Urusi, madai ambayo Tehran imekanusha.
Kwa hatua hizi mpya, Wairani watakuwa na ugumu zaidi wa kusafiri kwenda Ulaya. karibu mashirika yote ya ndege ya kigeni tayari yamesitisha safari zao za ndege kwenda Tehran kwa sababu ya hali ya kikanda na vitisho vya mashambulio ya Israeli.
Shirika la ndege la Flydubai pekee ndilo linaloendelea na safari zake za ndege. Kwa hiyo wasafiri wanaotaka kwenda Ulaya wanalazimika kwenda nchi jirani, ama Uturuki, Falme za Kiarabu au Qatar, kuchukua ndege kuelekea Ulaya.
Vikwazo hivi vipya vinafanya mazungumzo kati ya Tehran na nchi za Ulaya kuwa magumu zaidi, mazungumzo ambayo tayari yamedhoofishwa kwa sababu ya sera ya kikanda ya Iran, lakini pia mpango wake wa nyuklia na balestiki.