Jamshid bin Abdullah, Sultani wa mwisho kuitawala Zanzibar na aliyeondolewa madarakani kwa mapinduzi ya tarehe 12 Januari mwaka 1964 amefariki dunia.
Jamshid amefariki dunia katika hospitalini iliyopo nchini Oman jioni ya jana Jumatatu, Disemba 30 akiwa na umri wa miaka 95.
Taarifa za kifo chake zimeripotiwa na vyombo mbalimbali vya Habari nchini Oman.

Sababu za kifo zinaelezwa kuwa ni maradhi ya muda mrefu na uzee na anatarajiwa kuzikwa leo jumanne katika makaburi ya kifalme jijini Muscat, Oman.
Jamshid alichukua madaraka ya Usultani mnamo Julai mosi mwaka 1963. Miezi mitano baada ya kutawazwa kuwa Sultani baada ya Zanzibar kupata uhuru wake kutoka kwa Waingereza mnamo Disema 1963.
Hata hivyo, uhuru huo haukukubaliwa na wananchi wote visiwani Zanzibar, na kusababisha mapinduzi ya Januari 12 1964 ambayo yalitamatisha utawala wa Jamshid ambaye alikaa madarakani kwa miezi sita tu.
Baada ya kupinduliwa kwa serikali ya kisultani, Jamshid alikimbilia uhamishoni, awali nchini Oman ambapo hakupewa hifadhi na hatimaye alielekea nchini Uingereza.
Jamshid alizaliwa visiwani Zanzibar mnamo Septemba 16, 1929 na kupata elimu yake ya msingi visiwani humo na baadae aliendelea na masomo nchini Misri na hatimaye Uingereza ambako baada ya msomo alihudumu katika jeshi la wanamaji la nchi hiyo kwa takriban miaka miwili.

Alirejea Zanzibar katika miaka ya mwisho ya utawala wa babu yake Sultani Sayyid Khalifa. Baba yake Jamshid, Sultan Abdullah bin Khalifa alitawala kutoka Oktoba 1960 mpaka Julai 1963 alipofariki na kiti chake kurithiwa na Jamshid.
Jamshid alikuwa Sultani wa mwisho kuitawala Zanzibar na kabla yake walitawala masultani wengine 12. Sultani wa mwanzo akiwa Sayyid Said, ambaye alihamisha makao makuu yake kutoka Muscat Oman hadi Zanzibar mwaka 1840. Sayyid Said alikuwa Sultani wa Oman na Zanzibar kwa wakati mmoja.
Baada ya kufariki kwa Sayyid Said mwaka 1856, kukatokea ugomvi wa Madaraka baina ya wototo zake wawili Majid na Thuwain. Chini ya makubaliano yaliyosimamiwa na Waingereza, wakaigawa dola ya baba yao katika nchi mbili.
Majid akawa Sultani wa Zanzibar na Thuwain akawa Sultani wa Omani.
Japo utawala wa familia hiyo ya Busaidi ulikomeshwa visiwani Zanzibar Januari 1964 kwa kupinduliwa kwa Jamshid, nchini Oman bado familia hiyo inaendelea kutawala.
Moja ya masharti aliyopewa Jamshid aliporejea nchini Oman mwaka 2020 ni kuwa arejee kama mwanafamilia ya kifalme lakini si kama Sultani.