You are currently viewing Tamasha la Kizimkazi kuibua fursa za uchumi wa buluu

Tamasha la Kizimkazi kuibua fursa za uchumi wa buluu

Kizimkazi ni miongoni mwa maeneo yenye uwezo mkubwa wa kukuza uchumi wa buluu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kutokana na rasilimali zake za bahari, fukwe na mazingira ya kipekee ya ukanda wa pwani, hali inayofungua fursa za uwekezaji zinazoweza kuongeza ajira, kipato cha wananchi na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.

Miongoni mwa fursa hizo ni uvuvi wa kisasa, ambapo wawekezaji wanaweza kutumia teknolojia bora kuongeza uzalishaji wa samaki na mazao mengine ya baharini, kuboresha maisha ya wavuvi na kuimarisha upatikanaji wa chakula.

Kilimo cha mwani pia ni eneo lenye fursa kubwa za uwekezaji kupitia kuongeza uzalishaji, uchakataji na utengenezaji wa bidhaa za viwandani, dawa na vipodozi, hatua inayoweza kufungua masoko mapya na kuongeza thamani ya zao hilo.

Kizimkazi pia ina nafasi ya kuvutia uwekezaji katika huduma za usafiri wa baharini, ikiwemo boti za abiria na mizigo, pamoja na usindikaji wa mazao ya bahari unaoweza kuongeza thamani ya bidhaa, kukuza biashara na kutengeneza ajira kupitia uzalishaji, ufungashaji na usafirishaji.

Kwa kutumia rasilimali zake za bahari kwa njia endelevu, Kizimkazi ina uwezo wa kuwa kitovu muhimu cha uchumi wa buluu na kutoa fursa kwa wawekezaji pamoja na wananchi, huku fursa hizo zikipewa msukumo kupitia Tamasha la Kizimkazi litakalofanyika Agosti 12–14, 2026 litakalokuwa jukwaa la kuwakutanisha wadau, wawekezaji na wananchi kujadili na kuonesha nafasi ya eneo hilo katika kuinua uchumi wa buluu.

Katika tamasha hilo lenye kaulimbiu “Kizimkazi Kumenoga: Shangwe na Fursa,” kutakuwa na mdahalo wa uchumi wa buluu utakaolenga kujadili matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, uwekezaji na namna ya kuongeza manufaa kwa jamii.