ULIMWENGU wa soka imepatwa na huzuni baada mshambuliaji wa Kimataifa wa Ureno na Klabu ya Liverpool ya England, Diogo Jota (28), kufariki dunia katika ajali mbaya ya gari.
Kaka yake mshambuliaji huyo wa Ureno, Andre Silva (26) pia alifariki katika ajali hiyo iliyotokea katika jimbo la Zamora nchini Uhispania. Silva pia alikuwa mchezaji wa kulipwa, wa klabu ya daraja la pili ya Ureno ya Penafiel.

Taarifa rasmi kutoka kikosi cha jeshi la Hispania, Guardia Civil imesema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Rionegro del Puente, ambapo Kituo cha Zimamoto cha eneo hilo kilithibitisha kuwa ajali hiyo ilisababisha vifo vya vijana wawili wenye umri wa miaka 28 na 26.
“Gari hilo lilishika moto mara baada ya ajali na moto huo ukaenea hadi kwenye mimea ya jirani. Vijana hao walikuwa wamekwama ndani ya gari na walifariki papo hapo,” ilieleza taarifa ya Zimamoto.
Jota alianza kucheza soka katika nchi yake ya Ureno kupitia akademi ya Pacos de Ferreira kabla ya kujiunga na klabu ya Atletico Madrid ya Hispania mnamo mwaka 2016. Hata hivyo, hakuwahi kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo ya LaLiga, na badala yake alitolewa kwa mkopo kwenda FC Porto — klabu ya mji alikozaliwa — kisha akaelekea Wolverhampton Wanderers (Wolves) mwaka 2018.
Alitamba kwa misimu miwili akiwa chini ya kocha mwenzake wa Kireno, Nuno Espirito Santo, kabla ya kusajiliwa rasmi na Liverpool mnamo Septemba 2020.
Akiwa Liverpool, Jota aliibuka kuwa mmoja wa washambuliaji mahiri, akichangia mafanikio kadhaa ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England (Premier League), Kombe la FA na Kombe la Carabao. Pia alikuwa sehemu ya kikosi kilichofika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2021/2022, ambapo Liverpool ilipoteza dhidi ya Real Madrid kwa bao 1-0, Jota akicheza kama mchezaji wa akiba.
Jota aliitumikia timu ya taifa ya Ureno kwa mara ya kwanza mnamo Novemba 2019. Alishiriki michuano ya Euro 2020 na Euro 2024. Hata hivyo, alikosa Kombe la Dunia la mwaka 2022 kutokana na jeraha.
Kwa jumla, alifanikiwa kutwaa taji la UEFA Nations League mara mbili akiwa na kikosi cha Ureno, ikiwemo toleo la hivi karibuni lililomalizika Mei mwaka huu.