You are currently viewing  TANROADS yaagiza mameneja 26 kukagua barabara, madaraja kukabili El nino

 TANROADS yaagiza mameneja 26 kukagua barabara, madaraja kukabili El nino

Na Mwandishi Wetu

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amewaagiza Mameneja wa Mikoa yote 26 nchini kufanya ukaguzi wa kina wa barabara, madaraja, makalavati na maeneo hatarishi ili kubaini mapema changamoto na kuchukua hatua za kuzuia athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Mhandisi Besta ametoa agizo hilo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Ntyuka – Mvumi – Kikombo mkoani Dodoma, akisisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema ili kulinda mtandao wa barabara na kuhakikisha unaendelea kupitika kwa usalama wakati wa mvua.

“Natoa rai kwa Mameneja wote wa Mikoa 26 waende wakafanye ukaguzi na kuangalia ni namna gani wanaweza kupunguza athari zinazoweza kutokana na mvua za El Niño,” amesema.

Amesema hatua hiyo ni muhimu kutokana na changamoto zilizowahi kujitokeza wakati wa mvua, akitolea mfano Daraja la Mutikila, ambalo Desemba mwaka jana liliathiriwa na mvua na kusababisha usumbufu wa usafiri. Aidha, amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya kazi na kuhakikisha madaraja ya Mutikila, Mangungo na Kikombo pamoja na miundombinu mingine muhimu ya mradi inakamilishwa kwa wakati.

Kwa mujibu wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, mradi huo wenye urefu wa kilomita 76 unatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ya kilomita 25 imefikia asilimia 67.9. Kati ya hizo, kilomita 8.6 ziko Ntyuka kuelekea Mvumi, huku Kikombo ikiwa na kilomita 14.4, ikiwemo kilomita tano zinazounganisha barabara hiyo na barabara ya kuelekea Makao Makuu ya Jeshi.

Mhandisi Amani amesema mkandarasi ni CHICO, ambaye amekamilisha kilomita 23.2 kati ya 25 hadi kiwango kinachohitajika. Kazi zilizobaki ni pamoja na kujaza tuta la barabara, kuunganisha maeneo ya madaraja na kukamilisha miundombinu ya kupitisha maji katika Mutikila, Mangungo na Kikombo, pamoja na daraja la reli ya MGR.

Amesema TANROADS tayari imeanza kuimarisha maeneo hatarishi kwa kutumia kifusi, kuimarisha kingo za matuta na kufungua njia za mito, huku ikitarajia madaraja ya Mutikila, Mangungo na Kikombo kufikia hatua ya kupitika kabla ya kuanza kwa mvua.