You are currently viewing Tanzania, Marekani kuimarisha uhusiano

Tanzania, Marekani kuimarisha uhusiano

Tanzania na Marekani zimeonyesha dhamira ya kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, kukutana na Afisa Mkuu wa Masuala ya Kisiasa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Allison Hooker.

Katika kurasa za mitandao yao ya X (zamani Twitter) leo, Jumatano Juni 17, 2026, viongozi hao wamechapisha ujumbe kuonyesha wamekutana na kuzungumza kuhusu maendeleo ya ushirikiano wa pande mbili.

Kwa mujibu wa machapisho yao, miongoni mwa mambo waliyozungumza ni masuala ya ushirikiano wa biashara, uwekezaji, uhuru wa kuabudu na uhuru wa kujieleza, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza maslahi ya pamoja.

Allison kupitia chapisho lake la X, ameeleza dhamira ya Marekani kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kukamilisha makubaliano na miradi mbalimbali ya kibiashara yenye manufaa kwa wananchi wa mataifa yote mawili.

Waziri Kombo katika uwanja wa maoni wa mtandao huo, alilijibu chapisho la Allison kwa kuandika, mazungumzo hayo yamekuwa yenye tija na yameonesha utayari wa pande zote kuendeleza ushirikiano wa kimkakati utakaofungua fursa zaidi za maendeleo na uchumi.