You are currently viewing Tanzania, Singapore zasaini hati 5 za makubaliano ya ushrikiano

Tanzania, Singapore zasaini hati 5 za makubaliano ya ushrikiano

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Singapore, zimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano unaolenga kuimarisha uhusiano, kukuza biashara na uwekezaji.

Katika kufanikisha hilo, mataifa hayo yamesaini rasimu ya mikataba na hati tano za makubaliano ya ushirikiano, wakati wa ziara ya Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, aliyewasili nchini jana kwa ziara ya siku tatu Juni 8 hadi 10, mwaka huu

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo ya uwili kati ya Rais Shanmugaratnam na mwenyeji wake, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, viongozi hao wamesema wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali.

Dkt Samia, amesema ameikaribisha Singapore kufungua ubalozi wake nchini, pia wamekubaliana kuangalia njia za kukuza biashara na uwekezaji na uwezeshaji wa vijana hasa katika sekta ya uchumi wa kidigitali.

“Nimemweleza (Rais wa Singapore) dhamira yetu (Tanzania) ya kuwawezesha vijana katika elimu hasa ya ujasiriamali, ukuzaji ujuzi na ubunifu na Serikali imejielekeza zaidi katika uchumi wa kidigitali na kutekeleza mkakati wa uchumi wa kidigitali wa mwaka 2024/34,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake, Rais Shanmugaratnam, amesema pamoja na mambo mengine wamekubaliana kushirikiana katika mpango wa kukabiliana na magonjwa ya selimundu, uwekezaji katika kilimo na mazungumzo ya kufungua soko Huru la Afrika kupitia Umoja wa Afrika.

Katika hafla hiyo, mikataba mitano ilisainiwa ambayo ni, rasimu ya mkataba wa kuondoa utoaji kodi mara mbili na zuio la ukwepaji na uhepaji wa kodi

Mwingine ni rasimu ya hati ya makubaliano kati ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Wizara ya Mango ya nje ya Singapore, katika masuala ya uendelezaji ujuzi

Pia, rasimu ya hati ya makubaliano katika ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na Wizara ya Viwanda na Biashara ya Singapore, katika biashara za kabobi chini ya Ibara ya 6 ya mkataba wa Paris.

Mwingine uliosainiwa ni rasimu ya hati ya makubaliano ya mashauriano ya uwili kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Mambo ya Nje ya Singapore

Kadhalika, ilisainiwa rasimu ya hati ya makubaliano kati ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Taasisi ya Singapore katika masuala ya uwezeshaji wa biashara

Ziara hiyo ya Rais Shanmugaratnam, ni ya kihistoria na ya kwanza kufanywa na Rais wa Singapore nchini tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo, mwaka 1980.

Historia nyingine inayoandikwa katika ziara hiyo ni kwamba, inafanyika wakati ambao Tanzania na Singapore zinaadhimisha miaka 45 ya uhusiano wa kidiplomasia.

Rais Shanmugaratnam, anafanya ziara hiyo kwa siku tatu kuanzia Juni 8 hadi 10, mwaka huu. Ziara hiyo, inaendana na mkakati wa Tanzania wa kuimarisha diplomasia ya uchumi, ili kuvutia uwekezaji, teknolojia, masoko na utaalamu.