Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, wamekubaliana kuongeza kasi ya ushirikiano wa kiuchumi na biashara baina ya mataifa hayo mawili ili kufikia thamani ya biashara ya Dola za Marekani bilioni moja kwa mwaka.
Kwa sasa, Tanzania na Uturuki zinafanya biashara yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 354 kwa mwaka. Hivyo, viongozi hao wamezielekeza Serikali zao kuongeza juhudi za kukuza biashara na uwekezaji ili kufikia lengo hilo.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa, Novemba 13, 2026, na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dkt. Ng’waru Maghembe, muda mfupi baada ya kurejea nchini akitokea Uturuki, alikokuwa ameambatana na Rais Samia katika ziara yake.
Dkt Maghembe amesema viongozi hao wamezielekeza Serikali za nchi hizo mbili kuondoa vikwazo vya ushuru na vile visivyo vya ushuru vinavyoweza kukwamisha biashara.
“Wamezielekeza Serikali zote mbili kuondoa vikwazo vya ushuru na visivyo vya ushuru,” amesema Dkt. Maghembe.
