Tanzania imethibitisha kuendeleza ushirikiano wa kikanda ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakati maandalizi ya Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wa jumuiya hiyo yakifikia hatua za mwisho jijini Arusha.
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan tayari yupo Arusha kushiriki mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Machi 7, 2026, ukiwakutanisha viongozi wakuu wa nchi wanachama kujadili mustakabali wa ushirikiano wa kikanda.
Hatua hiyo inakuja katika kipindi ambacho jumuiya hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha za kuendesha shughuli za Sekretarieti ya EAC na mijadala kuhusu uongozi wa taasisi za jumuiya hiyo.

Kupitia ushiriki wake katika mikutano ya maandalizi, Tanzania inadhihirisha msisitizo wake wa umuhimu wa mshikamano wa nchi wanachama ili kuhakikisha ajenda ya ushirikiano inaendelea kusonga.
Maandalizi ya mkutano huo yamefanyika kupitia mnyororo wa mikutano ya kitaalamu na kisera, ulioanza na mkutano wa wataalamu Machi 2 hadi 3, 2026, ukafuatiwa na mkutano wa Makatibu Wakuu wanaosimamia masuala ya ushirikiano wa kikanda Machi 4, na kuhitimishwa na mkutano wa Baraza la Mawaziri wa EAC Machi 5.
Miongoni mwa masuala muhimu yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni maendeleo ya utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la EAC, kuondolewa kwa vikwazo visivyo vya ushuru katika biashara za kikanda pamoja na kufikiwa kwa mfumo endelevu wa michango ya nchi wanachama ili kuimarisha uwezo wa kifedha wa Sekretarieti ya jumuiya hiyo.
Viongozi pia wanatarajiwa kujadili na kuzindua Mkakati wa Saba wa Maendeleo wa EAC (2026/27–2030/31), ambao unalenga kuweka dira mpya ya maendeleo ya kiuchumi, kuimarisha biashara na uwekezaji pamoja na kuboresha miundombinu ya kikanda kwa manufaa ya wananchi zaidi ya milioni 300 wa Afrika Mashariki.
