You are currently viewing Tanzania yatinga nusu fainali CECAFA U20

Tanzania yatinga nusu fainali CECAFA U20

TANZANIA imefanikiwa kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA U20 baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Rwanda usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.

Hadi mapumziko Ngorongoro Heroes inayofundishwa na Kocha mkongwe, Charles Boniface Mkwasa anayesaidiwa na Kally Ongala na Juma Kaseja, Kocha wa makipa ilikuwa inaongoza 1-0, bao la winga wa Dodoma Jiji, Zidane Sereri dakika ya tatu.

Kipindi cha pili Ngorongoro Heroes ilirudi kwa nguvu zaidi na kufanikiwa kutanua ushindi wake kwa mabao ya winga wa KVZ ya Zanzibar, Sabri Dahari Kongo dakika ya 71 na 82.

Kwa ushindi huo, Ngorongoro Heroes inakamilisha mechi zake ikiwa na pointi tisa – ikishinda tatu, pamoja na dhidi ya Djibouti 7-0 na Sudan 1-0 baada ya kufungwa 2-1 na Kenya.

Ngorongoro wanaweza kushukia nafasi ya pili kama Kenya yenye pointi nne sasa itashinda mechi zake mbili zilizobaki na kama hawataweza kukusanya pointi kuipiku Sudan yenye pointi sita sasa wataikosa Nusu Fainali.

Tayari Kundi B limekamilisha mechi zake Uganda ikimaliza kileleni kwa pointi saba, ikifuatiwa na Burundi ambayo sasa ina pointi sita na zote zinafuzu Nusu Fainali.

Sudan Kusini imemaliza na pointi nne na Ethiopia wamehitimisha safari yao kinyonge baada ya kupoteza mechi zote tatu.

Bingwa na mshindi wa pili wa michuano hiyo watafuzu AFCON U20 ya mwakani.

Leave a Reply