HALMASHAURI ya Wilaya Magu kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) umegawa miche ya miti 13,059 kwa shule za sekondari Sukuma na msingi Magu kwa lengo kuendelea kuhamasisha upandaji miti na uhifadhi wa mazingira.
Zoezi hilo la ugawaji miti limezinduliwa leo Ijumaa na Katibu Tawala wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo katika eneo la bustani ya wilaya hiyo na kushuhudiwa na walimu pamoja viongozi wa taasisi mbalimbali ikiwamo za dini.
Akizungumza na wanafunzi hao baada ya kugawa miti hiyo Lawuo amewataka wanafunzi hao kuitunza miti hiyo ili kukabiliana na athari mbalimbali za mazingira.
“Hakikisha mti unakua ili utakapohitimu elimu yako mti huo utawasaidia wadogo zako wakae katika mazingira mazuri.
“Lakini pia miche ya miti ipo mingi hivyo nendeni kawaambieni pia wazazi waje wachukue miti ya matunda, kivuli na mbao,”amesema.
Naye Afisa Mhifadhi daraja la pili kutoka TFS wilaya ya Magu, Marwa Juma amesema zoezi la ugawaji au uzinduzi wa upandaji miti katika wilaya ya Magu linatokana na mchango wa serikali kwenye taasisi yao iitwayo Inkind Co financing kwa mwaka 2024/25.
“Mbali na kuendelea na zoezi la upandaji miti, lengo la taasisi hiyo ni uzalishaji miche 200,000 ambayo awamu ya kwanza ya ugawaji miche tayari imeanza.
Cleofasi Madaha ambaye ni mmoja wa walimu walioambatana na wanafunzi hao mbali na kuishukuru halmashauri kwa kupatiwa miti hiyo, pia ameahidi kuendelea kuwa mabalozi wa mazingira katika maeneo yao.
“Tunaishukuru wilaya imetutengeneza mazingira mazuri kupata miti hii, tunaahidi kwenda kuhamasisha jamii inayotuzunguka kupanda miti na kujali mazingira kwa sababu sisi ni mabalozi wazuri wa mazingira kwa ajili ya kutunza
Baadhi ya wanafunzi hao, Brian Francis Diana Godfrey kiutoka Sukuma sekondari na msingi, wameishukuru wilaya kupatiwa miti hiyo na kuahidi kuitunza hadi ikue.