You are currently viewing Uchumi wa Tanzania bado imara

Uchumi wa Tanzania bado imara

Ripoti ya Taasisi ya kimataifa ya tathmini ya kiuchumi, Moody’s Ratings, imesema Tanzania ni Taifa lenye uchumi unaokua kwa kasi na unaoaminika katika masoko ya fedha ya dunia, kunakoiwezesha kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI).

Wawekezaji mara nyingi hutafuta mazingira thabiti wanapowekeza mitaji yao. Kuimarishwa kwa kiwango na Moody’s rating  kunadhihirisha kuwa Tanzania inashughulikia changamoto zake kiuchumi kwa ufanisi, na hivyo kuwa mahali pazuri zaidi pa uwekezaji.

Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi ya kimataifa ya tathmini ya uwezo wa nchi kulipa madeni (Moody’s Ratings), Tanzania ina uwezo wa kulipa madeni yake kwa wakati licha ya kuwepo kwa changamoto za kawaida za kiuchumi (B1).

Kiwango hiki kinaonyesha tathmini yenye mizania kuhusu uwezo wa Tanzania kulipa madeni yake, ambayo inaweza kusaidia kujenga imani kwa wawekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi. Aidha inaonyesha kiwango thabiti kinavyoweza kuimarisha uwezo wa Tanzania kuingia kwenye masoko ya kimataifa ya mtaji.

Hii inamaanisha kuwa serikali inaweza kukopa kwa masharti bora zaidi, kuruhusu fedha kwa ajili ya miradi muhimu ya miundombinu kama vile barabara, shule, na hospitali. Kuboresha miundombinu hakika kunachochea shughuli za kiuchumi lakini pia kunaboresha maisha ya wananchi.

Sambamba na hilo hali ya uchumi wa Tanzania unatarajiwa kuendelea kuimarika na kukua kwa kwa kiwango cha asilimia 6, hali ambayo itaufanya uchumi kuwa imara zaidi.

Ripoti hiyo, inasema ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuwa zaidi ya asilimia sita, ukichangiwa na uwekezaji katika miundombinu, viwanda, madini na utalii.

Kwa upande wa mfumuko wa bei, umeendelea kubaki chini ya asilimia tano, jambo linalinda uwezo wa wananchi kununua bidhaa na huduma.

Kwa upande mwingine, Moody’s Ratings imesema bado kuna shinikizo la kijamii, linalochochewa na kipato duni cha wananchi na ongezeko la vijana wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.

Hata hivyo, ripoti hiyo inasema hatua za mageuzi ya kisera na mikakati zinazoendelea kuchukuliwa katika kushughulikia mambo hayo, zinaiweka Tanzania katika matarajio ya kuendelea kukua.

Leave a Reply