WANANCHI wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa ujenzi wa daraja la Sukuma, kwani litasaidia kuimarisha shuhuli za kiuchumi, kurahisisha usafirishaji na kurahisisha huduma nyingine za kijamii.
Hayo yameelezwa leo Machi 10,2026 na wananchi hao wakati Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenan Kihongosi alipotembelea mradi wa ujenzi wa daraja huo uliotekelezwa na serikali kwa zaidi ya Sh bilioni 9.4.

Kihongosi ametembelea mradi huo akiwa katika mwanzo wa ziara yake mkoani Mwanza na kuagiza daraja hilo kufunguliwa Aprili mwaka huu.
Wakizungumzia mradi huo mmoja wa wananchi hao Emmanuel Sabuni, amesema nyakati za mvua ilikuwa changamoto kwao, baadhi walilazimika kuvuka kwa mashaka na hofu, huku baadhi yao wakikumbana na adha ya kusombwa na maji.
“Kuna nyakati mifugo ipo kule (upande wa pili) mvua imenyesha kubwa huwezi kurudi, unabaki huko huko ulipo, wale waliolazimisha wengi wao walisombwa na maji,” amesema na kuungwa mkono na mwananchi mwingine Klango Nsabi ambaye amesema;
“Kipindi cha nyuma watu walikuwa wakisombwa na maji nyakati za mvua, wengine shindwa kuvuka na kukata mawasiliano ya Vaya na watu wanaokwenda wilayani.”
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa ujenzi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania, (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Ambrose Pascal, amesema daraja hilo la urefu wa mita 70 na ujenzi umefikia asilimia 80.
Amesema miongoni mwa kazi zilizofanyika ni ujenzi wa nguzo za katikati (Piers), kuta za mwanzo (Abutments), nguzo mlalo, Deck Slab na tabaka la changarawe.
Kihongosi ameanza ziara mkoani Mwanza na leo Machi 10, 2026 alipokewa na mamia ya wananchi katika Kijiji cha Masanza Nsola, wilayani Magu na kuwapa salamu za Rais Samia Suluhu Hassan.
