Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema kuwa ujenzi wa mejengo 36 ya serikali umefikia asilimia 89.4 huku Jengo la Wizara hiyo likiwa limekamilika kwa asilimia 95.
Msigwa amesema hayo alipotembelea majengo hayo yaliyopo Mtumba jijini Dodoma leo Februari 07, 2025 ambapo amesema hadi kukamilika ujenzi huo wa majengo 36 itagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 738 huku mpaka sasa zikiwa zimetumika shilingi Bilioni 457.
Katika hatua nyingine, Msigwa ameeleza kuwa, baada ya kukamilika kwa majengo hayo, awamu itakayofuata ni ujenzi wa miundombinu ya kudumu ikiwemo Hospitali, maeneo ya michezo, maduka makubwa, maeneo ya Kupumzikia, nyumba za ibada, nyumba za makazi, vyuo, sehemu za kitamaduni na barabara zenye urefu wa Kilomita 51.2.
Vilevile Msigwa amesisitiza kuwa miundombinu ya umeme, maji, mawasiliano, Tehama na usalama inayojengwa chini ya Ardhi, uboreshaji wa mandhari na bustani sambamba na ununuzi wa samani kwa ajili ya majengo hayo ukiwa unaendelea.
Aidha, Msigwa amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa majengo hayo, huku akieleza kuwa kukamilika kwa ofisi hizi kutawezesha watumishi kufanya kazi mahali pazuri na kwa ufanisi zaidi.
Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Marchi mwaka huu huku majengo matatu ikiwemo la Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala bora, na Wizara ya Maji yakiwa yamekamilika na yameanza kutumika.