You are currently viewing Utekelezaji  mradi wa ‘BOLD’ wavutia wadau sekta kilimo

Utekelezaji  mradi wa ‘BOLD’ wavutia wadau sekta kilimo

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Wadau mbalimbali wa maendeleo katika sekta ya kilimo hapa nchini wameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ‘Biodiversity for Opportunities, Livelihoods and Development’ (BOLD), unaolenga kuinua sekta ya mbegu kwenye nchi zaidi ya 50 duniani ikiwemo Tanzania, kupitia tafiti zinazoendelea kufanyika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti pembezoni mwa warsha inayoendelea ya wadau wa mnyororo wa thamani wa rasilimali za vinasaba vya mimea inayofanyika kwenye Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (World Vegetable Center)  jijini hapa, wameelezea kufurahishwa na utekelezaji wa mradi huo.

Mratibu wa mradi huo kutoka  Global Crop Diversity Trust (Crop Trust), Bw. Benjamin Kilian amesema mradi huo utakuwa mkombozi kwa wakulima wadogo, kwani  umebeba malengo saba  yatakayo leta matokeo endelevu kwenye tafiti za mbegu sambamba na kuongeza uzalishaji na uchakataji wa mazao yaliyosahaulika.

“Miongoni mwa malengo ya mradi huu ni pamoja na  kuimarisha uwezo na rasilimali, kuwezesha upatikanaji wa utofauti mpya wa  mbegu,  kuunganisha mabenki ya mbegu , wakulima na  mifumo ya mbegu,  kuhifadhi nakala salama katika hifadhi ya mbegu ya dunia ya Svalbard pamoja na  kuongeza uzalishaji na uchakataji wa mazao yaliyosahauliwa na yanayotumika kidogo  Barani Afrika,” alieleza Bw.  Kilian.

Bw. Kilian aliongeza kuwa siku tano, watashiriki pia katika vikao vya ushirikiano, mijadala ya sera, na ziara za shambani ili  suluhisho za pamoja  zinazoweza kutekelezeka kwa mifumo ya chakula imara na jumuishi.

“Mradi huo  unakwenda kuleta mapinduzi makubwa   hususani  katika kuboresha miundombinu na vifaa, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi kuhusu uendeshaji wa benki ya vinasaba, kuweka mfumo wa usimamizi wa ubora sambamba na kushirikisha makundi ya watumiaji,” alisema ba kuongeza kuwa pamoja na kuwahusisha wazalishaji wa awali, wakulima, maafisa ugani, watafiti na wadau wengine katika sekta ya mbegu.

Aidha Bw. Kilian aliipongeza Taasisi yaWorldVeg kwa kuwakutanisha pamoja wadau katika sekta ya  kilimo, na kubainisha kuwa  wamekuwa wakisaidia benki za kitaifa za vinasaba duniani kote, na Tanzania ni miongoni mwa washirika wao wakubwa.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Taifa  cha Hifadhi ya  Nasaba za Mimea  kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Dkt. Mujuni Sospeter Kabululu alisema  kwa upande wa Tanzania,  wanashiriki katika  vifurushi vitatu vya kazi  kati ya vile saba, kwa kuangalia jinsi watakavyoimarisha mifumo  ya mbegu, mifumo ya uhifadhi katika mazao manne  ambayo ni zao

ulezi, njugumawe, viazi vitamu na moringa.

“ Mazao haya yalichaguliwa kupitia  kikao cha wadau tulichokaa kuchagua ni aina gani ya mazao yaingizwe kwa ajili ya kuyafanyia tafiti pamoja na kuongeza matumizi yake,” alisema Dkt. Kabululu.

Alisema  kupitia mradi huo, kituo kimepiga hatua kubwa  kwani wamepata  vifaa vya maabara pamoja na vifaa vya  kuimarisha mifumo  ya uhifadhi wa taarifa za nasaba za mimea  pamoja na kuongeza uhusiano wao  na wadau wote wanaohusika na uhifadhi na matumizi endelevu za nasaba za mimea.

Naye Mkurugenzi Mkaazi wa  WorldVeg, Bi. Colleta Ndunguru alisema  wamekuwa na wasaa mzuri  kwani mradi huo umeweza kuwaweka pamoja  wataalamu zaidi ya 40  kujadili namna bora ya kuhifadhi nasaba za mimea pamoja na kuhifadhi mbegu za asili sambambana  kubadilishana uzoefu utakaochangia kukuza sekta ya mbegu duniani.

“ Tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na   wadau  wetu ambao ni Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) pamoja na  Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) katika kubadilishana  uzoefu na ujuzi   utakao tusaidia  kuzalisha mbegu zinazohimili magonjwa pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi,” alisema Bi. Ndunguru.

Naye Dkt.  Adolf Saria  kutoka TOSCI,  alisema  mradi huo utasaidia kuhakikisha mbegu ambazo zimesahaulika hususani  mbegu za mazao ya mboga mboga, ambazo mara nyingi hazifanyiwi utafiti wa kutosha na vinasaba vyake havitumiki na watafiti wa ndani katika kuzalisha mbegu bora, mbegu hizo zinahifadhiwa na  na kutumika kwenye tafiti, ili kuboresha aina za mbegu mpya  ambazo zitamnufaisha mkulima.

“  Sisi kama TOSCI tutahakikisha mbegu zinakidhi viwango vya kitaalamu vya ubora wa mbegu, ili ziweze kusaidia wakulima kwani wanazipenda ni mbegu zao  muda mrefu, ziingie  kwenye utaratibu mzuri ambao zinaweza zikazalishwa  kwa wingi ili nao wakulime wanufaike na mbegu hizo,” alisema Dkt Saria.

Mradi huo  unafadhiliwa na serikali ya Norway na kutekelezwa na ‘Crop Trust’  chini ya wabia wake katika nchi zaidi ya 50 duniani.

WWF

Leave a Reply