You are currently viewing Wabunge wakunwa ujenzi vituo maalum vya kudhibiti wanyama wakali

Wabunge wakunwa ujenzi vituo maalum vya kudhibiti wanyama wakali

Na Mwandishi Wetu, Tanga

Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza kilio cha wananchi kuhusu wanyama wakali na waharibifu na kuwajengea vituo na kutoa vifaa vya kukabiliana na changamoto hiyo  katika maeneo mbalimbali nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) ametoa shukrani na pongezi hizo wakati kamati hiyo leo Februari 17, 2024 ilipokuwa ikitamatisha ziara yake ya siku 3 katika Mkoa wa Tanga  kukagua mradi mbalimbali ambapo leo imekagua  ujenzi wa kituo maalum cha kukabiliana na tembo kilichokamilika kwa asilimia 100 katika kijiji cha Goha kata ya Mkumbara, wilayani Korogwe.

“Tumeridhishwa na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Rais wetu kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii katika kukabiliana changamoto hii katika kipindi kifupi, kwa niaba ya kamati naomba nimshukuru na kumpongeza sana” amesisitiza Mhe. Mnzava

Kituo hicho ambacho kimetumia  milioni 48 kukamilika  pia Serikali imetoa vifaa yote muhimu  ikiwa ni pamoja na samani, ndege nyuki 1, gari 1 na askari sita ambao watakuwa  kituoni hapo wakati wote.

Kituo hicho ambacho kina vyumba vikubwa 3, Ofisi moja, jiko, bafu na choo kitasaidia kukabiliana na changamoto hiyo katika vijiji zaidi ya kumi vinavyovunguka  eneo hilo.

Baadhi ya vijiji vitakavyofaidika moja kwa moja na kituo hiki ni pamoja na Manga, Mtitiro, Masira, Kwenangu, Mkomazi na Mikochen imeeleza taarifa ya Hifadhi ya Ngorongoro, taasisi ambayo imepewa jukumu la kujenga na kusimamia.

Aidha, Mnzava ameitaka Wizara kuhakikisha  mara baada ya kukamilisha vituo hivyo kuleta vifaa yote muhimu na watumishi wanaohitajika na wawepo muda wote.

Kamati hiyo iliambatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi, Naibu Katibu Mkuu, Kamishina wa Polisi, Benedict Wakulyamba na watendaji kutoka wizarani na kwenye taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.

Leave a Reply