Muungano wa wafanyakazi wa viwanja vya ndege nchini Kenya (KAWU) umesitisha mgomo wake ulioanza Jumatatu baada ya maafikiano na wizara ya uchukuzi nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA), makubaliano yao yanajumuisha kurejeshwa mara moja kwa shughuli katika uwanja wa ndege wa JKIA na pia kushughulikia matakwa ya wafanyakazi wa viwanja vya ndege.
Kumalizika kwa mgomo huo ulioanza Jumatatu kunatoa ahueni kubwa kwa wasafiri waliokuwa wamekwama katika uwanja wa JKIA, kutokana na safari zao kucheleweshwa au kuahirishwa.
Wafanyakazi hao wa viwanja vya ndege wamekuwa wakigoma kudai malipo bora na mazingira bora ya kazi.
Uwanja wa JKIA nchini Kenya ni kiungo muhimu barani Afrika, kwani unatumika sana kuunganisha safari mbalimbali za dunia na hutoa huduma kwa wasafiri zaidi ya Milioni 900 kila mwaka.
