Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro wametembelea Bandari ya Moroni kujione shughuli zinazofanywa hapo hususan katika kushughulikia shehena za mizigo kutoka Tanzania.
Wakiongozwa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Saidi Yakubu watumishi hao walipata fursa ya kufanya mazungumzo na Bw. Fahari Ibrahim, Meneja wa Bandari ya Moroni kutembelea ghala za kuhifadhia mizigo ya Tanzania na pia kushuhudia meli mbili toka Tanzania zikishusha mizigo yake mingi ikiwa ni bidhaa za chakula, vinywaji na samani.

Watumishi hao pia walizungumza na baadhi ya wasafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na Comoro wakieleza changamoto zao, ikiwemo meli kukosa muda wa kutosha kushusha mizigo, na wabebaji kutumia muda mwingi kuhudumia meli kutokana na kukosekana vitendeakazi muhimu.
Bandari ya Moroni hupata takriban meli 10 kwa mwezi toka Tanzania.
Balozi na Ujumbe wake walibaini umuhimu wa kusaidia kuongeza ufanisi katika Bandari hiyo kwa kupatiwa vitendeakazi muhimu, na kuimarisha mazingira ya ghala za kuhifadhia mizigo.