Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Vurugu kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imesema muda wa siku 21 iliyoongezewa unalenga kutumika kukamilisha kazi na sio kuchakachua ripoti kama inavyopotoshwa na baadhi ya watu.
Taatifa kuhusu tume hiyo kuongezewa muda imetokewa Aprili 4, 2026 kupitia Gazeti la Serikali, ikisema muda huo wa siku 21 ulioongezwa utatumika kukamilisha maandalizi ya ripoti na taarifa zilizokusanywa.
Hata hivyo, hii si tume ya kwanza kuwahi kupewa muda wa nyongeza kukamilisha kazi, ilifanywa hivyo hata na Tume ya Marekabisho ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba, iliyoongezewa miezi sita na baadaye miwili.
Mbali na Tanzania, Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Afrika Kusini ilipewa muda wa kuifanya kazi kwa miaka miwili Desemba 1995 hadi 1997, lakini ikaomba kuongezewa miezi sita na baadaye ikaomba sita mingine.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Chande Othman, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu sababu ya kuongezewa kwa muda huo.
Aidha, Jaji Chande amesema kuwa awali walipanga kufanya uchunguzi katika mikoa sita lakini wamelazimika kufikia mikoa 12 na kukusanya taarifa mfano kwanini Arusha kuwe na ghasia kubwa halafu Kilimanjaro zisiwepo, au Zanzibar kuwe shwari lakini Dar es salaam kuwe na ghasia wakati maeneo hayo yapo karibu.
Amesisitiza tume hiyo haiingiliwi, wala haina madalali bali inafanya kazi zake kama chombo huru.
