Na Mwandishi Wetu
Benki ya Dunia (WB), imeipongeza Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa usimamizi mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na taasisi hiyo.
WB imeitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa mataifa yanayoitekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi katika bara la Afrika.

Pongezi hizo zilitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkazi wa WB anayemaliza muda wake nchini, Nathan Belete, alipokutana na Dkt Samia Ikulu ya Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Belete amesema “miradi ya Tanzania ndani ya Benki ya Duniani ni miongoni mwa inayotekelezwa vizuri barani Afrika. Fedha zinazotolewa kwa Tanzania zinatumika vizuri na kuleta matokeo,” ameeleza.
Belete amesema katika kipindi chote alichofanya kazi Tanzania, ushirikiano kati ya Serikali na WB umeendelea kuimarika katika sekta mbalimbali zikiwemo za elimu, afya, maji, nishati, miundombinu, hifadhi ya jamii na mageuzi ya kisera.
Rais Dkt Samia amemshukuru Belete kwa mchango wake tangu alipoanza majukumu yake Novemba 2022, akisema ushirikiano wake umeendelea kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na WB katika kusukuma mbele ajenda za maendeleo.
Dkt Samia amesema,” Kwa sasa Tanzania inatekeleza programu na miradi 18 kwa ushirikiano na Benki ya Dunia katika sekta za usafirishaji, nishati, maji, elimu, maendeleo ya miji, hifadhi ya jamii, mageuzi ya kisera na ustahimilivu wa tabianchi,” amesema Dkt Samia.
