Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Chama cha Mawakili wa Serikali hakipaswi kuwa chanzo cha migogoro na migawanyiko ndani ya Taifa letu bali kuendeleza misingi ya amani, umoja na mshikamano nchini.
Amesema matarajio ya wananchi ni kuona chama hicho, kikitekeleza majumuku yake kwenye uelekeo wa misingi ya amani umoja na mshikamano nchini, hivyo wasikubali taaluma yao kutumika kuhalalisha jambo lisilo sahihi na lenye nia ovu dhidi ya Taifa.
“Ulimwengu wa sasa hivi, kila kitu, kila nguvu inatumika ili wenye nguvu kutimiza matakwa yao. Kuna nguvu ya fedha inazunguka duniani ili wenye nguvu kutimiza matakwa yao, niwaombe sana sisi ni Watanzania, Tanzania ni yetu sisi, si mtu mwingine,”
“Ikiendelea kuwa nzuri ni yetu, tukiivuruga na kuharibika ni yetu.
Narudia msemo niliowaambia wenzenu tutasaidiwa kuiharibu, lakini hatutasaidiwa kuijenga tena,” amesema Samia.
Dkt Samia amewataka mawakili na maofisa wa sheria wa Serikali kuchapa kazi kwa kutanguliza masilahi ya Taifa mbele huku wa Tanzania ndio nyumbani kwao, hakuna mahali pengine hivyo kilichopo nchini kilindwe.
