Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, wameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa nishati na kuifanya Tanga kuwa kitovu cha nishati cha kikanda.
Utiaji saini huo umefanyika leo Agosti 6, 2026 Ikulu, Dar es Salaam. Hati ya makubaliano iliyosainiwa ni kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Mafuta la Uganda (UNOC), pamoja na kampuni ya kimataifa inayojihusisha na nishati na biashara ya bidhaa ghafi, Vitol Bahrain E.C ya nchini Uholanzi.

Makubaliano hayo yanaendana na jitihada za kuimarisha nafasi ya Tanzania katika sekta ya nishati kupitia miradi ya kimkakati ikiwemo Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), linalounganisha maeneo ya uzalishaji wa mafuta ghafi Hoima nchini Uganda na Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Mradi wa EACOP unalenga kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi kwenye masoko ya kimataifa kupitia Bandari ya Tanga, huku ukiwa na umuhimu mkubwa katika kukuza biashara, uwekezaji, ajira na maendeleo ya miundombinu katika nchi hizo mbili.
Kupitia utekelezaji wa EACOP na miradi mingine ya nishati, Bandari ya Tanga inatarajiwa kuimarika zaidi na kuwa kitovu cha kimkakati cha nishati kwa ukanda wa Afrika Mashariki, sambamba na kuongeza uwezo wa Tanzania kuhudumia mahitaji ya nishati ya kikanda.
