Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali imetangaza kulifuta Kanisa la Ufufuo na Uzima, linalomilikiwa na Askofu Josephat Gwajima, ikiwa ni siku moja tangu kiongozi huyo wa kiroho atangaze msimamo wake wa kuendelea kukemea vitendo vya utekaji na watu kupotea.
Sababu ya uamuzi huo wa Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa ni kile kilichoelezwa kanisa hilo limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.
“Chini ya Kifungu cha 17(b) na kifungu cha 2 cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 kama kilivyorekebishwa na kifungu cha 39(b) cha Sheria ya Marekebisho Mbalimbali ya Sheria Namba. 3 ya Mwaka 2019.

“Katika siku za hivi karibuni, kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, umeonekana ukiwa katika mimbari ya Kanisa la Glory of Christ Church @ Kanisa la Ufufuo na Uzima, ukitoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi. Vitendo hivi ni kinyume cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337na vinaweza kuhatarisha amani na utulivu nchini
“Kwa Mamlaka niliyopewa, Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia inafuta usajili wa Glory of Christ Church @ Kanisa la Ufufuo na Uzima, kuanzia leo tarehe 02 Juni 2025. Hivyo, unatakiwa kusitisha shughuli za Kanisa lako mara moja,” imesema barua hiyo na kuongeza;
“Chini ya kifungu cha 19(1) cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, Kanisa lina haki ya kukata rufaa juu ya uamuzi huu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia kwa Katibu Mkuu, ndani ya siku 21 kuanzia tarehe ya barua hii. Kwa Amri ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia.”