Zaidi ya asilimia 95 ya wafanyakazi walioshiriki katika ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) walikuwa Watanzania, hatua iliyowajengea wataalamu wa ndani ujuzi na uzoefu wa kutekeleza miradi mikubwa kwa viwango vya kimataifa.
Hayo yamesemwa leo, Agosti 22, 2026, na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, wakati akiwasilisha taarifa ya mradi huo kwa Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uzinduzi wa JNHPP mkoani Pwani.
Twange amesema uzoefu walioupata Watanzania kupitia mradi huo utawaongezea uwezo wa kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi, huku akibainisha kuwa hata mhandisi mshauri wa mradi alikuwa Mtanzania.
Amesema ushiriki wa wataalamu wa ndani umeonesha uwezo wa Watanzania katika kusimamia na kukamilisha miradi mikubwa, sambamba na kuwajengea uwezo wa kushiriki katika utekelezaji wa miradi mingine mikubwa ndani na nje ya nchi.
Twange amesema kwa sasa kituo hicho kina watumishi 161 wanaohusika na uendeshaji, matengenezo na usimamizi wa miundombinu na kuwa licha ya kituo hicho kutumia teknolojia ya kisasa, kinaendeshwa na kusimamiwa na Watanzania.
