KILIO cha uhaba wa maji katika katika kata tano za wilaya ya Magu mkoani Mwanza, kinatarajiwa kupata dawa baada ya mradi wa ujenzi wa Tenki la Maji Bujora lenye ujazo wa lita milioni tano kufikia asilimia 98.
Mradi huo unaotarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu, unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wakazi wakazi 75,000 katika maeneo ya Kata za, Bujora, Kisesa, Bukandwe, Bujashi na Igudija.
Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Magu ilipotembelea eneo la mradi kujionea utekelezaji wake.
Kamati hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Magu, Enos Kalambo imesema imeridhishwa na kiwango cha utekelezaji wa kazi katika mradi huo, ikisisitiza umuhimu wa kukamilisha hatua zilizobaki ili wananchi waweze kunufaika na huduma.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Miradi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Martin Sungeni amesema maandalizi yanaendelea kuelekea majaribio ya kuingiza maji kwenye tenki hilo mwezi Oktoba 2026.
Aidha, amefafanua kuwa baada ya ujenzi kukamilika, kazi itakayofuatia ni ulazaji wa mtandao wa usambazaji maji kutoka kwenye matenki kwenda kwa wananchi ili wapate huduma.
Tenki la Kisesa ni sehemu ya mradi mkubwa wa kimkakati wa ujenzi wa matenki matano ya maji katika maeneo ya Buhongwa, Fumagila, Nyamazobe, Kisesa na Usagara, wenye jumla ya ujazo wa lita milioni 31, sambamba na vituo viwili vya kusukuma maji na kilomita 40.5 za mabomba makuu ya kusafirisha maji.
Mradi huo wenye thamani ya takribani Sh bilioni 46.2 unalenga kuimarisha usafirishaji na usambazaji wa maji kwa wananchi wa Mwanza na maeneo jirani ukitarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.
