Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) inashiriki Mkutano wa 12 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP 12) kuhusu usimamizi wa Mazingira ya Pwani ya Bahari ya Hindi, unaofanyika Jijini Dar Es Salaam ukijumuisha zaidi ya wajumbe 500 kutoka Nchi mbalimbali wanachama.
Mkutano huo, ambao umeanza Oktoba 6, 2026 unakutanisha Nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi ulio chini ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) huku ukilenga kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya ulinzi, usimamizi na uendelezaji wa mazingira ya bahari na ukanda wa Pwani katika kanda ya bahari ya Hindi ya Magharibi (WIO)
Miongozi mwa Viongozi waliopita katika banda hilo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Mheshimiwa Joel Nanauka ambaye amepongeza ushiriki wa DAWASA katika mkutano huo muhimu na kusisitiza elimu ya mabadiliko ya Tabianchi na athari zake kwenye sekta ya Maji ipewe kipaumbele kwa Jamii.
DAWASA ikiwa Moja ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maji inaonyesha shughuli zake sambamba na lengo la Mkutano huku ikionyesha utekelezaji wa miradi ya usafi wa Mazingira ya kimkakati wa Mbezi beach na Buguruni pamoja na mradi wa Bwawa la Kidunda unaolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
