Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imetangaza kusitisha kwa muda safari za ndege kati ya Dar es Salaam na Moscow, nchini Urusi, kuanzia Septemba 4, 2026.
Katika taarifa iliyotolewa Septemba 3, 2026, ATCL imesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kufanya tathmini ya kawaida ya hatari za kiusalama katika mazingira ya uendeshaji wa safari hizo.
ATCL imesisitiza kuwa usalama unaendelea kuwa kipaumbele chake kikuu kuliko masuala ya kibiashara, huku tathmini za mazingira ya uendeshaji zikiendelea kufanyika katika mtandao wake mzima wa safari.
Abiria waliokuwa na tiketi za safari zilizoathirika watapewa chaguo la kurejeshewa fedha zao kikamilifu au kupewa nafasi ya kusafiri katika tarehe au njia nyingine bila gharama ya ziada.
Kampuni hiyo imesema inaendelea kufuatilia hali ya usalama kwa kushirikiana na mamlaka husika na itatangaza kurejeshwa kwa huduma hizo mara tu tathmini itakapoonyesha kuwa ni salama kuendelea na safari.
ATCL imewaomba abiria kuwasiliana na kituo chake cha huduma kwa wateja au mawakala wao wa usafiri kwa maelezo zaidi.
