Jeshi la Madagascar limechukua madaraka kutoka kwa serikali ya kiraia baada ya Rais Andry Rajoelina kukimbia nchi, hatua iliyotangazwa na kamanda wa juu wa jeshi Kanali Michael Randrianirina mjini Antananarivo.
Rajoelina, ambaye awali aliingia madarakani mwaka 2009 kupitia mapinduzi yaliyoungwa mkono na jeshi, ameng’olewa madarakani baada ya wiki kadhaa za maandamano makubwa ya vijana waliopinga umaskini, kukatika kwa huduma za umeme na maji, na rushwa serikalini.
Ofisi ya rais imelaani hatua hiyo ikiiita uvunjaji mkubwa wa utawala wa sheria, ikisisitiza kuwa taifa bado limesimama. Lakini Kanali Randrianirina alisisitiza kuwa jeshi limeamua kubeba wajibu na kuunda baraza la kijeshi litakalosimamia serikali ya mpito.

Harakati zilizomng’oa Rajoelina zilianza kama maandamano madogo ya vijana waliopinga kukatika kwa umeme na maji, kabla ya kugeuka kuwa vuguvugu kubwa lililoungwa mkono na vyama vya wafanyakazi na mashirika ya kiraia.
Kundi la vijana wanaojiita “Gen Z Madagascar” limekuwa kiini cha maandamano hayo, likiiga mavuguvugu kama hayo yaliozitikisa Nepal na Sri Lanka.
Umoja wa Mataifa umesema takriban watu 22 waliuawa katika ukandamizaji wa awali uliofanywa na vikosi vya usalama, ingawa serikali ilipinga idadi hiyo.
Jumamosi iliyopita, majeshi ya CAPSAT yaliamua kujiunga na waandamanaji, yakidai Rajoelina ajiuzulu. Wakati wa mapambano na askari wa ulinzi wa serikali, mwanajeshi mmoja wa CAPSAT aliuawa, jambo lililoongeza hasira ya umma.
Mnamo Jumanne, wanajeshi walionekana wakiwa katika magari ya kivita wakishangiliwa na wananchi waliokuwa wakipunga bendera mitaani. Jeshi lilisema litaunda baraza linalojumuisha maafisa wa jeshi na polisi, litakalomteua waziri mkuu kuunda serikali ya kiraia “haraka iwezekanavyo.”
CAPSAT ndilo jeshi hilo hilo lililoshiriki katika mapinduzi ya mwaka 2009 yaliyomuweka madarakani Rajoelina. Wachambuzi wanasema kuna mfanano wa kihistoria kati ya matukio hayo mawili, kwani yote yamechochewa na hasira za wananchi dhidi ya utawala wa muda mrefu.
Ripoti zinasema Rajoelina alisafirishwa nje ya nchi kwa ndege ya kijeshi ya Ufaransa, jambo lililozua mjadala kuhusu nafasi ya taifa hilo la zamani la kikoloni katika kumpa hifadhi.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, akiwa Misri, alisema hatathibitisha wala kukataa taarifa hizo lakini alisisitiza urafiki wa Paris kwa watu wa Madagascar.
Rajoelina, ambaye anasemekana pia kuwa na uraia wa Ufaransa, amekuwa akikabiliwa na upinzani mkali wa kisiasa kutokana na uraia huo pacha.
Madagascar, licha ya utajiri wake wa vanila na urithi wa kiikolojia, imekuwa ikikumbwa na umaskini mkubwa na misukosuko ya kisiasa tangu ilipopata uhuru mwaka 1960.