You are currently viewing Kabila ahukumiwa kifo kwa kosa la usaliti

Kabila ahukumiwa kifo kwa kosa la usaliti

Mahakama ya kijeshi nchini Kongo- DRC imemhukumu kifo aliyekuwa rais Joseph Kabila baada ya kumtia hatiani kwa usaliti na uhalifu dhidi ya binadamu.

Chama chake PPRD kimesema kesi hiyo ni ya kisiasa dhidi ya mpinzani mkubwa wa serikali.

Hukumu hiyo imetolewa jana Jumanne na Luteni Jenerali Joseph Mutombo Katalayi, aliyesimamia shauri hilo katika mji mkuu Kinshasa.

Jaji huyo alisema Kabila, mwenye umri wa miaka 54, amepatikana na hatia katika mashtaka yanayojumuisha usaliti, mauaji, unyanyasaji wa kingono, mateso na uasi.

Kabila, ambaye aliitawala DRC kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, aliondoka nchini humo mwaka 2023.

Hata hivyo, mwezi Mei mwaka huu alionekana kwa muda mfupi katika maeneo ya mashariki ya nchi hiyo yanayodhibitiwa na waasi wa M23.

Kwa sasa haijulikani alipo baada ya hukumu hiyo ya mahakama ya kijeshi. Mwendesha mashtaka alimshtaki Kabila kwa kuunga mkono waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao mwaka huu wametwaa maeneo makubwa ya mashariki yenye utajiri wa madini.

Kesi yake ilianza kusikilizwa bila ya yeye kuwepo tangu Julai.

Waendesha mashtaka walisema Kabila alijenga uswahiba na M23 kwa lengo la kuipindua serikali ya Rais Felix Tshisekedi na kurejesha ushawishi wake wa kisiasa.

Kabila, kwa upande wake, amewahi kulaani mashtaka hayo akiyaita “kesi ya maigizo” na kuushutumu mfumo wa mahakama nchini kwa kuwa “chombo cha ukandamizaji”.

Aliongeza kuwa kesi dhidi yake, pamoja na kukamatwa kwa maafisa waandamizi wa kiraia na kijeshi, ni ishara ya kile alichokiita mgogoro wa uongozi, haki na mwelekeo wa taifa.

Chama chake, People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD), kimesema hukumu hiyo ni uwindwaji wa kisiasa na njama ya kumwondoa mpinzani mkubwa wa serikali.

“Wote wanajua kuwa hukumu ya Rais wa heshima Joseph Kabila Kabange ilishapangwa na serikali ya sasa. Kinachoendelea ni maigizo tu,” alisema katibu wa chama hicho, Emmanuel Ramazani Shadary.

Leave a Reply