Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba, amesema kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia kilichozindualiwa leo Julai 10, 2026, kina mchango muhimu katika taaluma ya sheria na uongozi.
Amesema kinadhihirisha namna uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ulivyoendelea kuimarisha misingi ya utawala wa sheria, haki, uwajibikaji, maridhiano, ushirikishwaji wa wananchi na maendeleo jumuishia.
Katimba ameyasema hayo leo Julai 10, 2026, wakati wa Uzinduzi wa Kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia uliofanyika katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM).
Amesema ni jambo la kujivunia kuona wataalam wakitumia taaluma zao kufanya tafakuri na uchambuzi unaochangia kujenga hazina ya maarifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka mazingira yanayokuza misingi ya sheria kupitia maboresho ya sheria, sera na mifumo mbalimbali ya utoaji haki.
Aidha, amesema Wizara ya Katiba na sheria inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, elimu ya sheria na huduma za msaada wa kisheria kupitia Msaada wa Kisheria wa Mama Samia Awamu ya Pili.
