You are currently viewing Maandalizi ujenzi kiwanja kipya cha ndege Serengeti yaiva

Maandalizi ujenzi kiwanja kipya cha ndege Serengeti yaiva

Maandalizi ya awali ya ujenzi wa Kiwanja Kipya cha Ndege cha Kimataifa cha Serengeti yameanza rasmi, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa usafiri wa anga nchini na kurahisisha upatikanaji wa utalii katika eneo hilo maarufu.

Mradi huu unakusudiwa kuwezesha ndege za kimataifa kufika moja kwa moja katika hifadhi hiyo, kupunguza muda na gharama za usafiri kwa watalii.

Hivi karibuni Bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ilitembelea eneo la mradi ili kukagua maendeleo ya maandalizi, ukaguzi wa usanifu wa kiwanja, mipango ya utekelezaji, na kuhakikisha kila hatua ya awali inafanywa kwa mujibu wa viwango vinavyohitajika.

Ziara hiyo pia ililenga kuthibitisha hali ya eneo, ukubwa wa mradi, na maandalizi ya kimkakati kabla ya kuanza rasmi kwa ujenzi. Ujenzi wa kiwanja hiki unalenga kuimarisha fursa za utalii na biashara za kimataifa huku kiwanja hiki kipya kikitarajiwa kurahisisha usafiri wa moja kwa moja ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kupunguza muda na gharama za safari, na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la utalii wa kikanda na kimataifa.

Leave a Reply