Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
MAGARI mawili yaliyotolewa bandarini yakielekea bandari kavu (ICD) Vingunguti, Dar es Salaam, yanadaiwa kubadilishiwa mwelekeo na kupelekwa Kigamboni, tukio lililosababisha watu saba kufikishwa mahakamani wakikabiliwa na shtaka la wizi.
Washitakiwa hao ni Isack Gerald Natus, Samson Mwamoto, Daniel Noah, Adam Sufian, Michael Wambura Marwa, Fadhil Arumia Munisi na Tusho Kalambire.
Wote saba wamefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Victoria Mwaikambo, na kusomewa shtaka hilo ambalo wamelikana.
Akisoma maelezo ya shtaka, Wakili wa Serikali, Nicas Kihemba, amedai kuwa washitakiwa hao waliiba magari mawili, moja aina ya Nissan Caravan na lingine Toyota Regiusace yaliyokuwa yametolewa bandarini kwa ajili ya kupelekwa ICD Vingunguti.

Magari hayo yanatajwa kuwa mali ya Sudais Logistic Company Limited.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, badala ya magari hayo kufikishwa katika ICD yalipokuwa yakipelekwa, mwelekeo wake ulibadilishwa na kupelekwa Kigamboni.
Inadaiwa kuwa Agosti 12, 2026, operesheni maalumu ya kudhibiti wizi wa magari na vifaa vinavyotolewa bandarini kwenda ICD mbalimbali iliwafikisha maofisa katika nyumba ya Michael Wambura, ambako magari hayo mawili yalikutwa.
Kukamatwa kwa magari hayo kulisababisha washitakiwa saba kutiwa mbaroni kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Baada ya washitakiwa wote kukana shtaka, upande wa Jamhuri uliieleza mahakama kuwa kesi hiyo itaendelea katika hatua nyingine za kisheria.
Hakimu Mwaikambo ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 26, 2026, itakapotajwa tena.
Washitakiwa wote wako nje kwa dhamana.
