ABIRIA waliokuwa wakisafiri kuelekea Nairobi na Entebbe kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kisumu nchini Kenya jana Jumatatu walikwama kwa muda mrefu huku shughuli usafiri wa angani zikitatizwa.
Mgomo wa Muungano wa Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege (KAWU) ambao unaingia siku yake ya tatu leo ndio ulisababishia abiria kadhia hiyo ya safari.
Wafanyakazi hao walianza tena mgomo Jumamosi usiku kutokana na malalamiko mbalimbali, yakiwemo yale yaliyosababisha kusimamishwa kwa mgomo wa awali mwezi uliopita.
Mwenyekiti wa KAWU, Walter Ongeri aliwaambia wandishi wa habari kuwa wafanyakazi waliamua kurejea kwenye mgomo baada ya serikali kushindwa kutekeleza masharti ya mkataba wa maelewano (MoU) uliotiwa saini na muungano huo.
“Tulitia saini makubaliano ya kurejea kazini lakini, kwa bahati mbaya, KAA na KCAA zimeshindwa kushughulikia malalamiko yetu. Asasi hizo mbili hazijajitolea kikamilifu katika mazungumzo na zimeshindwa kushirikiana nasi katika kutafuta suluhu ya malalamishi yetu,” akasema Katibu Mkuu wa KAWU Moss Ndiema.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini Kenya (KAA) ilisema viwanja vya ndege kote nchini vilikumbwa na kadhia ya abiria kucheleweshewa safari.
“KAA inashirikiana kwa karibu na mashirika husika ya anga, kampuni za ndege na wadau wengine kudhibiti hali hiyo, kupunguza usumbufu na kuhakikisha shughuli za viwanja vya ndege zinaendelea kwa utaratibu,” alisema.
KAA iliwashauri abiria kuwasiliana na kampuni zao za ndege kupata taarifa kuhusu safari zao.
Miongoni mwa waliokwama ni Kaimu Katibu wa Kaunti ya Siaya, Elizabeth Adongo, ambaye safari yake ya Safarilink kuelekea Nairobi ilisukumwa mbele baada ya kukaa uwanjani kwa saa kadhaa.
“Ujumbe kutoka Safarilink ulifika karibu saa saba mchana ukisema safari ilikuwa imeahirishwa,” alisema.
Abiria mwingine, Lennox Omondi, mfanyakazi wa Serikali ya Kaunti ya Siaya, pia aliathiriwa na mgomo huo.
Usumbufu huo uliwaacha abiria wengi uwanjani, huku baadhi wakitafuta njia mbadala za kufika walikokuwa wakielekea.
Kufikia Jumatatu alasiri, uongozi wa Uwanja wa Ndege wa Kisumu ulikuwa katika kikao cha dharura kutathmini hali na kupanga hatua za kuchukua.
Baadhi walibaki uwanjani wakisubiri taarifa kutoka kwa mashirika ya ndege na mamlaka ya nyuga za ndege, huku wengine wakiachana na mipango ya kusafiri kwa ndege na kutumia mabasi.
