Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinapaswa kutumika kutatua changamoto za wananchi na kuboresha maisha yao.
Akizungumza leo, Novemba 2, 2026, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi wateule iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Rais Samia amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Angelina Mabula, kusimamia kwa umakini matumizi ya fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Rais Samia amesema uzoefu wa Mabula katika nyadhifa mbalimbali za uongozi, zikiwemo Mkuu wa Wilaya, Naibu Waziri, Waziri na Mbunge, unampa uelewa mpana kuhusu majukumu ya Serikali, namna fedha zinavyotengwa na mahitaji ya wananchi.
Aidha, ametaka ushirikiano kati ya viongozi na watumishi wa Serikali kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi ili kuleta manufaa kwa wananchi na kutatua changamoto zinazowakabili.
