RAIS Samia Suluhu Hassan ameipongeza Yanga Sc. kwa kufanikiwa kutetea taji lake la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya nne mfululizo baada ya kuishindilia Simba SC. goli 2-0.
Yanga imefanikiwa kutwaa taji hilo baada kufikisha pointi 82 na kuiacha Simba ikiwa na alama 78 baada ya kukamilisha duru ya michezo 30 ya ligi kuu kwa msimu huu.
Kwa hatua hiyo leo Jumatano Yanga imemaliza msimu kwa kishindo cha kuibuka na ushindi mnono wa mabao 2-0 dhidi ya wapinzani wao wakubwa, Simba SC, katika dabi ya Kariakoo iliyosubiriwa kwa hamu.

Mchezo huu wa 184, ambao umekuwa gumzo la msimu kutokana na kuahirishwa mara mbili na kujaa maswali mengi, hatimaye umepigwa na kutoa majibu yote yaliyokuwa yakisubiriwa.
Licha ya ukimya na kutokuwepo kwa shamrashamra za kawaida zilizotangulia dabi hii, Yanga wameonyesha ubabe wao uwanjani na kuthibitisha ubingwa wao.
Kabla ya mchezo, ulimwengu wa soka ulitawaliwa na maswali mengi kuhusu hatma ya dabi hii, kutokana na historia yake ya kuahirishwa na malalamiko ya “ukulwa na doto” katika ligi.
Hata hivyo, baada ya vikao vya ngazi za juu vilivyojumuisha viongozi wa timu zote mbili na Rais Samia Suluhu Hassan, mambo yalianza kubadilika.