Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema atahakikisha amani na utulivu vinatawala katika msimu wote wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Katika kauli yake hiyo, amewasihi wananchi kufuata utaratibu uliowekwa wa kupiga kura na kurudi nyumbani, kwa kuwa uchaguzi ni tendo la kidemokrasia na sio vita.
Dkt Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumatano Septemba 17, 2025 alipozungumza na wananchi wa Makunduchi visiwani Zanzibar, wakati wa mkutano wake wa kampeni za urais, alioufanyia katika Uwanja wa Kajengwa.
“Uchaguzi ni tendo la kidemokrasia, ni watu kwenda kwa utaratibu uliowekwa, kuweka kura zetu rudi nyumbani katulie ili nchi ibaki salama,” amesema.
Amewataka wananchi visiwani humo, kuhakikisha katika uchaguzi wanadumisha amani na utulivu, kwani tukio hilo sio tendo la vita.
Dkt Samia amesema baada ya kuapishwa kuwa Rais, alikutana na wazee wa Pemba, pamoja na mambo mengine walimwelekeza kuhakikisha anadumisha amani na utulivu, jambo ambalo ameapa kuhakikisha linatimia.
“Si muda wote kushika silaha kunaleta suluhisho, muda wote kushika silaha yoyote, iwe ya moto au ya kimila hakuleti suluhisho la maana. Niwaombe sana wote wanaotusikiliza, amani na utulivu wa nchi yetu ni jambo la muhimu zaidi kuliko mengine yote hasa wakati huu wa uchaguzi,” amesema.
Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania, vimejipanga vema kulinda nchi.
“Sasa hutaki kishindo kapige kura rudi nyumbani tulia, tumejipanga vema. Kwa hiyo nisisitize suala la amani na utulivu,” amesema Dkt Samia.
Kauli hiyo ya Dkt Samia, imesisitizwa pia na Mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt Hussein Ali Mwinyi aliyesema amani, umoja, mshikamano na maridhiano nchini Tanzania kwa kuwa ndicho kipaumbele cha chama hicho.