Waziri wa michezo wa Nigeria, Seneta John Enoh ameagiza timu ya Super Eagles iliyokwama nchini Libya tangu Jumapili mchana kurejea nyumbani, akisisitiza kuwa ‘wasiwasi wa Serikali na watu wa Nigeria ni usalama wa timu na kurejea kwao salama.’
Katika taarifa yake kwenye akaunti ya mtandao wa X iliothibitishwa, Enoh alisema amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais na Katibu Mkuu wa CAF, ambao walielezea wasiwasi wao lakini akaomba timu iruhusiwe kucheza mechi iliyopangwa.
Alisema ‘Shirikisho la Soka la Nigeria limeagizwa kuwasilisha malalamiko rasmi kwa CAF bila kuathiri hatua zozote ambazo tayari zimechukuliwa,’ huku akitaka shirikisho hilo la soka barani kuchukua hatua dhidi ya Shirikisho la Soka la Libya.
Kufuatia kauli ya Enoh, Super Eagles sasa wanatarajiwa kuondoka Libya baada ya kukaa uwanja wa ndege kwa saa 16, wachezaji wakiachwa na machovu na kukosa la kufanya.
Wakati huo huo, Shirikisho la kandanda barani Afrika (CAF) limetoa taarifa likisema kwamba limekuwa na mawasiliano na mamlaka ya Libya na Nigeria baada ya kuarifiwa kuwa Timu ya Taifa ya Kandanda ya Nigeria (”Super Eagles”) na timu yao ya ufundi walikuwa wamekwama katika mazingira ya kutatanisha kwa saa kadhaa katika uwanja wa ndege ambao wanadaiwa kuagizwa kutua na mamlaka ya Libya.
Suala hilo limewasilishwa kwenye Bodi ya Nidhamu ya CAF kwa uchunguzi na hatua stahiki zitachukuliwa kwa waliokiuka Sheria na Kanuni za CAF.