You are currently viewing Trump ampa ulaji Elon Musk

Trump ampa ulaji Elon Musk

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump usiku wa kuamkia leo Jumatano ametangaza kuwa atamteua bilionea Elon Musk na mgombea urais wa zamani wa chama cha Republican, Vivek Ramaswamy kuongoza ldara mpya ya Ufanisi Serikalini (DOGE) pindi atakapoingia madarakani mwaka wa 2025.

Katika taarifa yake Trump amesema kuwa Musk na Ramaswamy watafungua njia katika uongozi wake, kuondoa urasimu Serikalini, kupunguza kanuni za ziada, kupunguza matumizi yasiyo na tija.

Trump alisema kazi yao wawili hao itakamilika ifikapo Julai 4, 2026 na kuongeza kuwa serikali ndogo na yenye ufanisi zaidi itakuwa zawadi kwa nchi hiyo katika maadhimisho ya miaka 250 ya kutiwa saini kwa Azimio la Uhuru.

Elon Musk ambaye ni mfanyabiashara bilionea na mmiliki wa Tesla, X (zamani Twitter), na SpaceX, pamoja na Vivek Ramaswamy, mgombea urais wa zamani wa Republican, wamekuwa wafuasi wa sera za Rais mteule Trump katika kipindi cha kampeni zake Musk amemuunga mkono Trump, akichangia mamilioni ya fedha katika kampeni zake na kuonekana hadharani na rais huyo wa zamani.

Aidha, Trump alikuwa ameeleza hapo awali kwamba angempa Musk nafasi kubwa katika utawala wake kusaidia kuendesha juhudi zinazolenga kuboresha ufanisi wa serikali pamoja na Ramaswamy.

Ramaswamy ambaye alishindana na Trump kwa uteuzi wa urais wa chama cha Republican mwaka 2024, alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho na baadaye kumuidhinisha rais huyo wa zamani.

Wote wawili watafanya kazi pamoja ili kurahisisha utendaji kazi wa shirikisho na kukuza ubunifu ambao utafanya serikali ya Marekani kuwa na ufanisi zaidi.

Leave a Reply